Askofu Ruwa'ichi aagiza  wakatoliki kufanya Novena siku tisa kuombea  'Haki na Amani' nchini

Askofu Ruwa'ichi aagiza wakatoliki kufanya Novena siku tisa kuombea 'Haki na Amani' nchini

PAROKIA na Asasi zote za Jimbo Kuu la Dar es Salaam, zimeagizwa kufanya Novena ya siku tisa kuanzia  Agosti 15, kwa ajili ya kuombea 'Haki na Amani' nchini

Agizo hilo limetokewa na Askofu  Mkuu 

wa Jimbo Kuu Katoliki  la Dar es saalam Mhasham sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi OFMCap.

Kufanyika kwa Novena hiyo ni utekelezaji wa agizo la  Askofu Ruwa'ichi alilolitoa Julai 7 mwaka huu wakati wa sherehe za Upadrisho zilizofanyika katika viwanja vya Msimbazi Center, jijini Dar es Salaam.

Novena hiyo ya kuombea Haki na Amani nchini imekuja kipindi ambacho Tanzania inajiandaa kuingia kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Kwa mujibu wa barua ya 'Canceller' wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam,  Padre Vicent Mpwanji kwenda kwa Maparoko, Madekano, Mapadre, Watawa na Walei wote,  Askofu Ruwa'ichi ameagiza Novena hiyo imeambatane na kuabudu Ekarist Takatifu, Rosari Takatifu na kusali sala ya kuiombea Tanzania kama ilivyotolewa na Baraza la Maaskofu nchini (TEC).

"Aidha katika siku ya kilele cha Novena hiyo yaani Agosti 23 kwa Kanisa la Tanzania, ndiyo siku ya kufunga na  kukesha katika kusali kwa ajili ya kuombea Haki na Amani nchini.

"Sote tunaalikwa  kufuata ratiba iliyotolewa na Idara ya Kichungaji ya TEC ambayo inaelekeza namna ya kufanya sala na mfungo huo ambao utaanza hiyo siku ya Agosti 23 kwa adhimisho la Ekaristi Takatifu, ikifuatiwa  na  Kuabudu Ekarist Takatifu, ikiambatana na vipindi mbalimbali vya sala, mafundsho na ukimya nakuhitimishwa Dominika Agosti 24 kwa adhimisho la Ekaristi Takatifu na inapendekezwa iwe misa ya kwanza kwenye makanisa yote," ilisomeka  sehemu ya barua hiyo.

Maelekezo ya Askofu Mkuu DSM.pdf