Askofu Mhashamu Sana Jude Thaddeus Ruwa'ichi akizindua nyumba ya mapadre na Tovuti ya Parokia
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddeus Ruwa'ichi OFMCap, amezindua nyumba mpya ya kisasa ya Mapadre wa Kanisa la Parokia ya Kung'ara kwa Yesu Kristo, iliyopo Mbezi Mshikamano.

Uzinduzi huo ulifanyika hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Msimamizi wa Kanisa hilo, Mt. Yohane Paul II.
Katika maadhimisho hayo Askofu Ruwa'ichi pia alizindua Tovuti (Website) pamoja na kuzindua Jubilee ya miaka kumi ya Parokia hiyo tangu ilipoanzishwa.
Akieleza histori fupi ya ujenzi wa nyumba ya mapadre ya ghorofa moja, Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Halmashauri ya Parokia ya Kung'ara Yesu, Adam Kamanda, alisema gharama za ujenzi wa mradi huo hadi utakapo kamilika 100 ni sh milioni 800.
" Hadi sasa ujenzi wa nyumba hiyo umefikia asilimia 95 na imejengwa na wakandarasi na fedha za waamini wenyewe kupitia michango yao", alisema Adam Kamanda.
Kwa mujibu wa Kamanda baada ya kukamilika kwa ujenzi wa nyumba ya mapadre, kazi inayofuata ni ujenzi wa Goroto ya Mama Bikira Maria na ukumbi wa Parokia, hivyo alimwomba Askofu Ruwa'ichi kwamba wakati ukifika, asisite kuja kuzindua.
Matukio mengine yaliyofanywa na Askofu Ruwa'ichi kwenye maadhimisho hayo ni utoaji wa Sakramenti ya Kipaimara, Sakramenti ya Ndoa za pamoja na uwekaji wa masalia ya Msimamizi wa Parokia, Mtakatifu Yohane Paulo II katika Altare ya Kanisa.
Jumla ya waumini 46 walipata Sakramenti ya Kipaimara na jozi nane za waumini walifunga ndoa za pamoja na kupata chakula cha mchana na Askofu Ruwa'ichi.